Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Wanajeshi 40 wengi wao wa vyeo vya juu wa Uturuki waliokuwa wakifanya kazi katika kambi ya Jeshi la kujihami la nchi za magharibi NATO nchini Ujerumani ambao walifukuzwa baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki mwezi Julai mwaka jana wameomba hifadhi nchini Ujerumani. Gazeti la Der Spiegel na kituo cha matangazo cha ARD vimeripoti hapo jana. Hakuna maelezo yaliyopatikana mara moja kutoka serikalini au maafisa wa NATO. Taarifa za wanajeshi hao wa Uturuki kuomba hifadhi ya kisiasa zinakuja mnamo wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akijiandaa kuzuru Uturuki ambako atakuwa na mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdogan. Mahusiano kati ya mataifa hayo mawili washirika wa NATO yamezorota kutokana na masuala mbalimbali likiwemo ujerumani kuwatuhumu wahubiri wa kidini wa kituruki kufanya upelelezi nchini Ujerumani pamoja na Ujerumani kutoafikiana na operesheni inayoendeshwa na serikali ya Uturuki ikilenga kuwatia mbaroni wapinzani wa kisiasa nchini humo. Aidha Uturuki imekuwa ikiishutumu Ujerumani kwa kuwapa hifadhi wanamgambo wa chama cha wafanyakazi kilichopigwa marufuku nchini humo cha PKK. Norbert Roettgen kiongozi wa kamati ya bunge ya mambo ya nje alilieleza gazeti la Spiegel nchini Ujerumani kuwa suala la kisiasa halitatumika katika kushughulikia maombi hayo ya visa.
Mwisho wa habari/ 291